Luke 6:20-49

Baraka Na Ole

(Mathayo 5:1-12)

20 aAkawatazama wanafunzi wake, akasema:

“Mmebarikiwa ninyi mlio maskini,
kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu.
21 b Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa,
kwa sababu mtashibishwa.
Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa,
kwa sababu mtacheka.
22 c Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia,
watakapowatenga na kuwatukana
na kulikataa jina lenu kama neno ovu,
kwa ajili ya Mwana wa Adamu.
23 d “Furahini na kurukaruka kwa shangwe, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.

24 e “Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri,
kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu.
25 f Ole wenu ninyi mlioshiba sasa,
maana mtaona njaa.
Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,
maana mtaomboleza na kulia.
26 g Ole wenu watu watakapowasifu,
kwani ndivyo baba zao walivyowasifu
manabii wa uongo.

Wapendeni Adui Zenu

(Mathayo 5:38-48)

27 h “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. 28 iWabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. 29 jKama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyangʼanya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. 30 kMpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie. 31 lWatendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.

32 m “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwapenda wale wawapendao. 33Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo. 34 nTena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. 35 oLakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. 36 pKuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

Kuwahukumu Wengine

(Mathayo 7:1-5)

37 q “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. 38 rWapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

39 s Pia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni? 40 tMwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake.

41 u “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? 42 vUtawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, acha nitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako,’ wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako? Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.

Mti Na Mazao Yake

(Mathayo 7:16-20; Marko 12:33-35)

43 w “Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri. 44 xKila mti hujulikana kwa matunda yake. Kwa maana watu hawachumi tini kwenye miiba, wala zabibu kwenye michongoma. 45 yVivyo hivyo mtu mwema hutoa mambo mema kutoka kwenye hazina ya moyo wake, naye mtu mwovu hutoa mambo maovu kutoka kwenye hazina ya moyo wake. Kwa kuwa mtu hunena kwa kinywa chake yale yaliyoujaza moyo wake.

Mjenzi Mwenye Busara Na Mjenzi Mpumbavu

(Mathayo 7:24-27)

46 z “Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia? 47 aaNitawaonyesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda. 48Yeye ni kama mtu aliyejenga nyumba, akachimba chini sana, na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, maji ya ghafula yaliipiga ile nyumba, lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri. 49Lakini yeye anayesikia maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi bila kuweka msingi. Mafuriko yalipoikumba nyumba ile, ikaanguka mara na kubomoka kabisa.”

Copyright information for SwhNEN